Tuesday, December 23, 2008

BAKHRESSA KUMLIPA FIDIA MOHAMED DEWJI SHS.739 MILLIONI

Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara, imeiamuru Kampuni ya Said Salim Bakhresa (SSB) kulipa fidia ya zaidi ya Sh milioni 739 kwa Kampuni ya Agro-Processing & Allied Product Ltd baada ya kutumia nembo yake katika biashara kimakosa. Kampuni ya Agro-Processing & Allied Product Ltd ilifungua kesi hiyo ya madai dhidi ya SSB baada ya kutumia nembo yake ya ‘Poa’ iliyokuwa ikitumiwa na kampuni hiyo na ambayo ilisajiliwa Machi 5, 2001 chini ya Msajili wa Nembo. Kampuni hiyo inadai kuwa kati ya Juni mwaka huohuo, mlalamikiwa naye alijaribu kusajili nembo yenye neno ‘Sembe poa’, ‘Unga poa’ na ‘Ngano poa’ na kutumia nembo hizo katika biashara zake. Mlalamikaji katika kesi hiyo ambaye ni Kampuni ya Agro- Processing & Allied Product Ltd, ilifungua kesi katika mahakama hiyo kwa kosa la kutumia nembo yake kufanyia biashara. Aliiomba mahakama iiamuru kampuni hiyo iilipe gharama zaidi ya Sh milioni 209 kama gharama halisi; kuondoa bidhaa zote zilizopo sokoni zenye nembo hiyo na kulipa gharama nyingine ambazo mahakama itaona zinafaa kulipwa. Jaji Bernard Luanda aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo, aliridhia ombi hilo la mlalamikaji baada ya kugundua kuwa SSB imefanya makosa kutumia nembo hiyo katika biashara zake. Aliamuru ilipe Sh milioni 50 kama gharama za hasara iliyoingia kampuni iliyolalamika na Sh milioni 80 kama adhabu kwa kampuni hiyo. Aidha, Jaji Luanda alisema kwa kuwa kampuni iliyolalamikiwa ilitumia nembo hiyo katika bidhaa zake kwa muda mrefu wakati si nembo yake, inatakiwa iilipe kampuni inayolalamika Sh milioni 400 kwa hasara iliyoisababishia kampuni hiyo kwa kipindi chote hicho iliyotumia kampuni hiyo.

No comments:

Followers