SPIKA wa Bunge la Muungano, Samwel Sitta ameongeza chachu katika mjadala wa kumuondolea kinga Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, baada ya kueleza kuwa yuko tayari kupokea na kujadili hoja binafsi za wabunge ili ikiwezekana kiongozi huyo wa serikali ya awamu ya tatu apandishwe kizimbani.
Tayari mawaziri wawili wa Mkapa, Basil Mramba na Daniel Yona, pamoja na katibu mkuu wa wizara, Gray Mgonja wameshafikishwa mahakamani kwa tuhuma za kutumia vibaya ofisi wakati wakiwa mawaziri, lakini bado baadhi ya watu wanataka rais huyo mstaafu apandishwe kizimbani kwa makosa aliyoyafanya akiwa Ikulu.
Mbunge wa Karatu, Dk Wilibrod Slaa ametangaza nia yake ya kuwasilisha hoja binafsi katika kikao kijacho cha Bunge la Muungano, kutaka Mkapa afikishwe mahakamani akidai kuwa suala hilo halihitaji kiongozi huyo wa zamani kuondolewa kinga kama wasomi walivyoshauri, huku kiongozi wa upinzani bungeni, Hamad Rashid akisema ameshaandaa hoja binafsi ya kumuondolea kinga Mkapa.
Na Spika Sitta alikuwa na maneno mazuri kwa wabunge hao wawili na watu wengine wanaoshinikiza kutekelezwa kwa suala hilo.
"Nitatilia maanani hoja yoyote inayomhusu Mkapa itakayofikishwa mezani kwangu na kuiruhusu ijadiliwe ndani ya Bunge," alisema Sitta.
"Bunge bado lina nafasi ya kujadili suala la Rais Mkapa na kulitolea maamuzi kama bunge... na wala mlango haujafungwa kuhusu hoja binafsi itakayotolewa, hivyo kama kuna mbunge yeyote mwenye hoja kuhusu suala hilo anaruhusiwa kuiwasilisha mezani kwangu siwezi kukataa kuipokea."
Lakini Spika Sitta akakumbusha utaratibu wa kuwasilisha hoja bungeni. "Kabla ya hoja hiyo kujadiliwa rasmi bungeni, kuna kamati ya uongozi ambayo hukutana na kuijadili na ikibainika kwamba hoja iliyowasilishwa imejitosheleza na inastahili kujadiliwa, hufikishwa mbele ya wabunge kwa ajili ya mjadala huo," alisema.
Spika Sitta alisema moja ya kanuni za bunge kuhusu hoja yoyote inasema kwamba "hoja lazima ijitosheleze na iwe na uhusiano na suala husika" na kama itajitosheleza kamwe hawezi kufungiwa mlango.
"Kwanza kabla ya mtoa hoja hajawasilisha hoja yake anatakiwa awe na mtandao na wabunge wenzake na wakubaliane ili iwe rahisi kwa hoja yake kuungwa mkono na wenzake bungeni na itakapobainika kwamba, hoja hiyo ina nguvu na imeungwa mkono na wabunge wengi, basi bunge linaweza kubadili katiba na hatimaye Rais huyo Mstaafu akashitakiwa kama raia yeyote ndani ya nchi,"alifafanua Sitta.
Spika Sitta aliongeza kuwa hatua ya pili ambayo mwasilisha hoja anatakiwa kuzingatia ni suala la kanuni za bunge, katiba ya nchi na sheria zilizopo na kwamba hayo yote yakitekelezwa na hoja ikajitosheleza kulishawishi bunge kufanya marekebisho ndani ya katiba yeye kama Spika ama mtu mwingine hawezi kupingana na maamuzi hayo ya bunge.
Alionya kuwa mtoa hoja asipozingatia mambo hayo badala yake akaamua kutoa hoja kwa jitihada zake binafsi huku akijiami kwamba, anaweza kulishawishi bunge kwa kutumia nguvu ya hoja zake, anaweza asifanikiwe hata kama kamati yake ya uongozi itaipitisha hoja hiyo.
Dk Slaa anasema suala la Mkapa kufikishwa mahakamani halihitaji kuondolewa kinga kwa maelezo kuwa tuhuma zinazomkabili za kufanya biashara akiwa Ikulu hazihusiani na nafasi yake kama rais bali mtu binafsi.
Lakini Rashid aliiambia Mwananchi jana kuwa ameshaandaa hoja hiyo na sasa anatafuta kuungwa mkono.
"Kwanza ninampongeza Dk Slaa kwa uamuzi wake wa kujiandaa kuwasilisha hoja hiyo... na mimi natarajia kwamba tutakapokutana na wabunge wenzangu, akiwemo Dk Slaa, tutajadiliana suala hilo ingawa nimeshamaliza kuandika hoja yangu kuhusu marekebisho ya katiba ili Mkapa aweze kushitakiwa pamoja mambo mengine ndani ya nchi kama vile marekebisho ya mikataba feki," alisema Rashid na kuongeza:
"Ili Rais ashtakiwe ama kuondolewa kinga, inabidi katiba ibadilishwe na hivyo ninaamini kwamba, kwa hoja zetu safari hii wabunge watazikubali hasa ikizingatiwa kwamba suala la Mkapa ni kilio cha wananchi cha muda mrefu."
Aliongeza kwamba katiba ina mapungufu mengi na moja ya mapungufu hayo ni kuwapa viongozi nguvu ya kutoshtakiwa na kwamba, katiba hiyo hiyo pia inajipinga yenyewe katika baadhi ya vipengele vyake.
No comments:
Post a Comment