Ndivyo unavyoweza kufupisha kitendo cha baadhi ya wabunge na wananchi wa mkoani Mtwara kujitokeza hadharani na kumtetea rais wa serikali ya awamu ya tatu, Benjamin William Mkapa.
Wakati shinikizao la kutaka Mkapa aondolewe kinga na kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma za makosa anayodaiwa kufanya akiwa Ikulu, wabunge na wananchi wa mkoani Mtwara na wananchi kuibuka na kumtetea.
Tayari mbunge wa Karatu, Dk. Wilbroad Slaa ameahidi kuwasilisha hoja ya kutaka Mkapa, aliyeongoza nchi kwa vipindi viwili (1995-2005), apandishwe kizimbani kujibu tuhuma za kufanya makosa wakati akiwa Ikulu, huku kiongozi wa upinzani Bungeni, Hamad Rashid, akiahidi kuwasilisha hoja ya kutaka kiongozi huyo aondolewe kinga ili aweze kupandishwe kizimbani.
Miongoni mwa tuhuma za Mkapa, ambaye anasifika kwa kuinua uchumi baada ya kuukuta kwenye hali mbaya, ni kujiuzia mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira mkoani Mbeya kwa bei nafuu akitumia kampuni ya Tan Power Resources anayoimulika pamoja na waziri wa zamani wa nishati na madini, Daniel Yona wakati akiwa rais.
Lakini wabunge hao na wananchi wa Mtwara wanaona kuwa tuhuma hizo dhidi ya Mkapa, ambaye alikuwa mbunge wa Nanyumbu wilayani Masasi kabla ya kuchaguliwa kuwa rais, hazitoshi kumuondolea mazuri yote aliyofanya wakati akiwa rais, kwa kuamua kumpandisha kizimbani kiongozi huyo aliyedumu miaka yote kumi ya urais wake akitumia sera ya "Uwazi na Ukweli".
"Huo ni upuuzi na nitaupinga kokote," alisema mbunge wa jimbo la Masasi, Raynald Mrope. "Siasa za sasa ni za kuchafuana... watu wanafikiri wakimchafua wenzao ndio wao watapata umaarufu.
"Jamani Mkapa amelitumikia taifa hili na kuliacha katika hali nzuri. Hata huyo Dk. Slaa tukisema tuchunguze upadre wake tutakuta makosa; binadamu hakosi kasoro ila muhimu tusiangalie alipoteleza tu, pale alipoweza mbona hatupasemi?"
Mbunge wa jimbo la Mtwara, Mohamed Sinani alizungumzia suala hilo kidiplomasia zaidi, lakini akashindwa kuficha msimamo wake kwa Rais Mkapa, ambaye aliteuliwa na CCM kuwania urais baada ya kumshinda Rais Jakaya Kikwete katika marudio ya kura za maoni.
"Sisi Wabunge tupo kwa ajili ya kuifanyia marekebisho katiba, kutunga sera na sheria," alisema Sinani na akaongeza kusema: "(Suala la hoja binafsi) Likiletwa tutalijadili, lakini pamoja na majukumu hayo sidhani kama ni busara kuifanyia marekebisho katiba kila kukicha, hasa pale unapomlenga mtu fulani.”
Mbunge wa Tandahimba, Juma Njwayo aliamua kutoweka bayana msimamo wake na akazungumzia suala hilo kiufundi zaidi, akisema ni mapema mno kulizungumzia na kwamba anasubiri kwanza liwasilishwe kama hoja binafsi Bungeni.
"Ndugu yangu hili suala ni la Kikatiba, tusubiri walete hoja na vielelezo vya ushahidi, tutalijadili kuona uzito wake.Wakati huo ukinipigia (simu) nitakuwa katika nafasi nzuri ya kutoa maoni yangu, kwa sasa ni mapema mono," alisema Njwayo aliyehojiwa kwa njia ya simu.
Baadhi ya wananchi wa mikoa hiyo walihojiwa na Mwananchi walionekana kupinga hoja hiyo, wakitaka Mkapa aangaliwe pia kwa mazuri aliyofanya.
"Mkapa aliichukua nchi ikiwa katika hali ngumu… mfumuko wa bei ulifikia zaidi ya asilimia 10, lakini ameuacha ukiwa katika asilimia 4.5. Si hilo tu amefanya mengi ambayo anastahili kuheshimiwa na kuachwa apumzike. Watanzania wenzangu tusiwe na shukrani za Punda," alisema Ibrahim Mchopa mkazi wa mjini Mtwara.
Alisema kutoka na utendaji aliouita kuwa mahiri wa Mkapa wakati wa uongozi wake, umewafanya Watanzania wengi kumuunga mkono hadi sasa na kwamba kitendo cha kumshitaki ni udhalilishaji ambao unaweza kuleta mgawanyiko katika umoja wa kitaifa uliopo.
"Leo hii tukisema wangapi wanamuunga mkono Mkapa tutawapata wengi kuliko wachache wanavyofikiri. Tunapomfikisha mahakamani kwa tuhuma ambazo msingi wake ni kutafuta umaarufu wa kisiasa, sidhani kama tunalitakia mema taifa hili," alisisitiza Mchopa.
Mkazi mwingine Rashidi Athuman alisema kuondolewa kwa kinga kwa marais waliomaliza muda wao kutasababisha machafuko ya kisiasa na hatimaye kuvunjika kwa amani na utulivu.
"Tunamshangilia Dk. Slaa, lakini kesho tutakuja kujutia. Ni lazima watu wawe na mtazamo wa mbali. Nilifurahi kumsikia Rais Kikwete akisema hatamshitaki Mkapa, bila shaka aliona mbali. Kimsingi siungi mkono si tu kwa sababu Mkapa ni wa kusini bali alivyoliongoza taifa," alisema Athumani akimzungumzia Mkapa ambaye ni mzaliwa wa kijiji cha Lupaso wilayani Masasi.
Mkazi mwingine aliyetoa maoni alisema kwa kuwa sheria ni msumeno na kwamba ni matarajio yake kuwa kuondolewa kwa kinga hiyo haitakuwa kwa Mkapa, bali hata rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi na kwamba vinginevyo madai hayo yatakuwa yamelenga kumchafua Mkapa kisiasa.
"Nilivyoelewa mimi ni kwamba kinga ikiondolewa ni kwa marais wote waliomaliza muda wao kwa kuwa katiba ni moja. Hivyo kama Mzee Mwinyi naye alitenda kosa wakati wa utawala wake, basi atachukuliwa hatua. Hali kadhalika kwa rais wetu atakapomaliza muda wake, kama alitenda kosa naye atashitakiwa," alisema Mohammed Omari.
No comments:
Post a Comment