CHAMA cha NCCR-Mageuzi kimesema maandamano na migomo inayotokea nchini inasababishwa na serikali kushindwa kutatua kero za wananchi na kwamba hayasababishwi na chama chochote cha siasa.
Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu wa Habari na Uenezi wa chama hicho, David Kafulila alisema wanaosema Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kinachochea vurugu siyo kweli.
Kafulila alitoa kauli hiyo siku chache baada ya wanachama wa Chadema kuandamana mjini Mwanza, na baada ya siku mbili, Rais Jakaya Kikwete alihutubia taifa na kusema kwamba Chadema kinataka kuleta machafuko kwa kudai mambo yasiyotekelezeka.
“Kazi wanayoifanya Chadema sioni kama ina tatizo, mimi tunatofautina na Chadema, lakini si kwa kila jambo, wanaosababisha maandamano siyo Chadema, NCCR wala CUF ni wananchi kwa sababu serikali imeshindwa kutatua matatizo yanayowakabili,” alisema Kafulila.
Alisema iwapo wanafunzi vyuoni wangepata mikopo yao kwa wakati, wafanyakazi kulipwa mishahara mizuri pamoja na mambo mengine kutekelezwa kwa wakati hakuna Mtanzania ambaye angelalamika wala kuandamana.
“Tatizo la umeme sio la chama ni la wananchi, hata sisi NCCR tuko tayari kwa lolote, tutaanza kazi kama wanayoifanya Chadema, lengo letu sote ni kuhakikisha wananchi wanapata haki zao na si kupika chuki katika jamii,” alisema Kafulila.
Alisema licha ya Tanzania kuwa nchi ya saba duniani kwa kupata misaada, lakini kila kukicha inazidi kurudi nyuma kimaendeleo.
“Tanzania ni ya saba kwa kupewa misaada, halafu wananchi wakiandamana vinasingiziwa vyama vya siasa kuwa ndio chanzo,”alisema.
“Hatuipingi Chadema, siipingi Chadema, NCCR tunajipanga kuwasha moto kuamsha watanzania waiwajibishe serikali yao, pale inaposhindwa kutatua matatizo bila sababu,” alisema Kafulila
No comments:
Post a Comment