Wednesday, January 07, 2009

Ujasiriamali kuchangia kuinua maisha ya vijana kiuchumi

Mafunzo ya ujasiriamali, yakiwekewa mazingira bora, yaweza kuwakomboa vijana wengi kiuchumi na kuwafanya waache kujiingiza kwenye vitendo vya kihuni. Ukosefu wa mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana wengi nchini yaweza kuwa unachangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la vitendo vya uhalifu na uharibifu wa mazingira nchini kwa hiyo kama kutakuwa na msukumo mpya huenda mambo yakawa tofauti. Utafiti unaonyesha kuwa, asilimia kubwa ya vijana hasa wale wanaoishi mijini hawana ujuzi wowote unaoweza kuwafanya wajitegemee kwa kuendesha maisha yao, na kuepuka kujitumbukiza katika janga la uhalifu. Serikali na baadhi ya mashirika yameanza kuchukua hatua kadhaa za kurekebisha hali hiyo. Hatua hizo ni pamoja na kuwaunganisha vijana katika makundi na kuwapatia mikopo kwa ajili ya kujiendeleza. Utoaji wa mikopo waweza kuwa si wa maana sana kama vijana hawatapatiwa mafunzo ya ujasiriamali wa namna ya kujiendeleza. Baada ya kubaini tatizo hilo, shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na masuala ya utunzaji wa miji salama duniani lijulikanalo kama International Center for Sustainable Cities (ICSC), limeamua kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa makundi ya vijana jijini Dar es Salaam bila gharama yeyote. Mafunzo hayo yametolewa kwa kushirikiana na halmashauri ya jiji la Dar es Salaam (DCC) kwa makundi ya vijana kwa lengo la kuwafanya wajitegemee na kuacha uhalifu. Mafunzo hayo yatawasaidia vijana wanaoishi jijini Dar es Salaam kupata ujuzi wa kibiashara, hasa namna ya kuandika mapendekezo jambo
linaloonekana kuwa ndilo tatizo lao kubwa.

Moja ya dhumuni la mafunzo hayo yanayotolewa chini ya mpango wa miji salama ni kuifanya miji kuwa safi na salama. Kwa sasa, mpango huo unaofadhiliwa na serikali ya Canada. Unafanya kazi katika miji ya Dar es Salaam, Durban na Dakar. Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, afisa mradi wa ICSC ya Canada, Bi. Victoria Smith, anasema moja ya changamoto kubwa inayowakabili vijana katika nchi mbalimbali ni ukosefu wa elimu ya namna ya kufanya biashara. `Kama unavyojua vijana ndio asilimia kubwa ya idadi ya watu duniani. Wengi wao hawana kazi na bado hawajawekewa misingi imara, sisi tumeona kuna umuhimu mkubwa wa kuwapatia mafunzo hayo, ambayo yatawawezesha kuanzisha miradi midogo ya kujipatia kipato`, anasema. Shirika hilo, pia limedhamiria kutoa mikopo kwa vijana hao ambayo wataitumia kama mtaji wa kuanzisha miradi midogo.

Mikopo hiyo itatolewa mara baada ya kutoa mapendekezo ya miradi kwenye shirika. Alidokeza kuwa, watachukua mapendekezo yote yaliyotolewa kwenye semina hiyo na kuyafanyia tathimini zaidi. Kwa upande wao, baadhi ya vijana waliohudhuria mafunzo hayo waliishukuru serikali ya Tanzania na ile ya Canada kwa msaada huo na kuomba msaada zaidi. Bw. Mohammed Busogoro wa shirika la Ilala Youth Development Society (IYODESO) anasema mafunzo hayo, yamewasaidia sana kupata ujuzi wa kibiashara ambao hawakuwa nao. `Tatizo la ukosefu wa ujuzi wa biashara ni changamoto kubwa sana kwetu, mafunzo haya yametufungua macho kwani tutayatumia ipasavyo kwa ajili ya maendeleo binafsi` anasema. Mafunzo hayo ya biashara anasema pia yatawasaidia kuanzisha biashara ndogo ndogo na kuendeleza zile zilizopo. Mjasiriamali huyo, ametoa wito kwa serikali kuwapatia vijana mikopo midogo itakayowasaidia kupambana na umasikini pia kuepukana na vitendo vya uhalifu.

Mjasiriamali mwingine aitwaye Fatuma Kazumari wa kikundi cha Tolabora, Temeke anasema, atatumia mafunzo hayo kuwaelimisha wenzake, ambao hawajayapata ili wajikwamue kuinua kipato chao. Anazishauri taasisi nyingine na serikali kuwapatia mikopo au vifaa vya kufanyia kazi. Mratibu wa Mpango ya Miji Salama wa Dar es Salaam, Bi Martha Mkupasi anasema kuwa, licha ya kuwapatia ujuzi, lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwawezesha vijana hao kujishughulisha na uzalishaji ili kuachana na vitendo vya uhalifu mpango huo unaangalia njia muafaka za kuweza kuwasaidia vijana hao kupigana na umasikini. Zaidi ya vikundi 19 vya vijana katika jiji la Dar es Salaam wamepata mafunzo ya ujasiriamali na wanatarajiwa kupewa mikopo kwa ajili ya kuanzisha biashara. Kuanzishwa kwa mafunzo hayo, kunatakiwa kuwa chachu kwa mashirika au kampuni nyingine zianzishe mipango ya aina hiyo kwa makundi mbalimbali ya jamii. Serikali kwa upande wake, haina budi kutoa ushirikiano wa pekee kwa makampuni yaliyoonyesha nia ya kusaidia maendeleo ya vijana.

Hatua muhimu ambayo inaweza kuchukuliwa ni kutoa dhamana za mikopo yenye riba nafuu au kupunguza kiwango cha kodi au kufuta kabisa kodi kwenye vifaa watakavyoomba vijana hao vinavyoagizwa kutoka nje kwa ajili ya kufanyia kazi zao. Hatua hiyo,yaweza kuwa ikachangia kuhamasisha vijana wengi kujiunga katika vikundi vya uzalishaji na kuachana na wazo la kufanya uhalifu kama njia mbadala ya kuinua uchumi.

No comments:

Followers