ASKOFU Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, amesema haoni tatizo katika maandamano yanayofanywa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi jana, Kardinali Pengo alisema badala yake Serikali: “Ichimbue mizizi ya matatizo badala ya kukimbilia kukata matawi.”
Kauli ya Pengo ni kama inaunga mkono matamshi yaliyotolewa juzi na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta ambaye aliishauri Serikali kutotumia vyombo vya dola dhidi ya Chadema na badala yake ijirekebishe kwa kuwa na wepesi wa kukabiliana na matatizo yaliyopo nchini.
Kadhalika, kauli hiyo ya Pengo imekuja wakati Serikali ikiendelea kulaani maandamano hayo ya Chadema na kutaka yasitishwe kwa madai kuwa yanaweza kuleta machafuko nchini.
Katika mahojiano hayo Kardinali Pengo alisema haoni kama Chadema kinafanya vurugu katika maandamano yake kama baadhi ya watu wanavyodai: “Sioni ‘point’ ya kusema maandamano ya Chadema yanaweza kusababisha vurugu,” alisema Kardinali Pengo na kuongeza:
Alisema ikiwa kuna tatizo katika maandamano hayo kama inavyoelezwa na serikali, ni bora hali hiyo ikafafanuliwa mapema na kukiambia Chadema kisitishe kuandamana.
“Lakini serikali isichukulie ‘comment’ (maoni) ya mtu mmoja mmoja na kusema kwamba Chadema inasababisha vurugu, bila kusikiliza na kuchambua kwa undani,” alisema.
Aliongeza kuwa endapo serikali imechunguza na kubaini ukweli kwamba maandamano hayo yanaweza kuleta vurugu za kisiasa, basi iyasitishe badala ya kutoa kauli tu kwamba yanahatarisha amani.
Pengo alisema huenda uamuzi wa Chadema kufanya maandamano unatokana na madai yao dhidi ya kupanda kwa gharama za maisha, umeme na malipo kwa kampuni ya kufua umeme ya Dowans kwamba hayakusikilizwa.
Alisema Serikali haitakiwi kuyafumbia macho matatizo ya kisiasa nchini badala yake itafute kiini chake na namna ya kuyatatua.
“Serikali ianze kuchimbua mizizi ya matatizo ya kisiasa yaliyopo ndani ya Taifa, badala ya kukimbilia kukata matawi. Kwa sababu kuanza kukata matawi ni kuzidi kuipeleka nchi katika machafuko ya kisisasa na matokeo yake ni kuleta madhara kwa wananchi,” alisema.
Askofu huyo mkuu pia alisisitiza kuwa Serikali inatakiwa kuhakikisha inafuatilia matatizo yanayowakabili wananchi kwa sasa, ambayo yanahitaji ufumbuzi wa haraka ili watu wasipate fursa ya kudai mambo hayo kwa maandamano.
Kwa mujibu wa Kardinali Pengo, Serikali pia haipaswi kutoa vipaumbele kwenye masuala ya siasa na kusahau matatizo ya wananchi kwani hilo linaweza kuwa kiini cha vurugu... "Serikali iguswe kama ilivyoguswa na matokeo ya mtihani wa kidato cha nne yaliyotoka mwaka huu."
Baadaye akihubiri katika Misa ya Jumatano ya Majivu kuashiria kuanza kwa siku 40 za Mfungo wa Kwaresma ambao Wakristo hukumbuka mateso ya Bwana wao, Yesu Kristo kabla ya Pasaka zaidi ya miaka 2000 iliyopita, Kardinali Pengo alikemea tabia ya viongozi kung'ang'ania madaraka na kudhani kuwa bila wao nchi zao haziwezi kuwepo au kusonga mbele.
"Yapo matatizo katika viongozi wanaong'ang'ania madaraka wakiwa tayari hata kumwaga damu ya wengine ili wao wabaki madarakani. Hawa ni viongozi wanaofikiri uwezo unaweza kuwa ndani yao, wanajifanya wao Mungu," alisema Pengo.
Alisema viongozi hao wanatazama fadhila za kibinadamu wakiacha upungufu wao na kudhani kuwa wasipokuwa na madaraka basi nchi zao hazitakuwepo jambo ambalo si sahihi na halifai katika jamii.
"Viongozi hao wanajifanya wao ndiyo miungu, wanatazama fadhila za kibinadamu, wakiacha mapungufu yao. Hicho ni kiburi, wakumbuke kuwa Mungu aliwaumba kwa vumbi na watarudi kuwa vumbi, sasa kwa nini mnakuwa na kiburi?," Alihoji Kardinali Pengo na kuongeza;
"Mungu aliwaumba kwa vumbi kwa nini wawe na kiburi? Unadhani ukifa na nchi itakufa, kwani kabla yako nchi haikuwepo? Kumbuka wewe ni uvumbi na utarudi mavumbini."
Alisema thamani ya mtu haitokani na anavyojiona, bali nguvu ya Mungu akiwakumbusha Wakristo kutubu na kumrudia Mungu katika kipindi hiki cha Kwaresma.
Wakati huohuo; Festo Polea anaripoti kuwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam ambao wapo katika taasisi isiyo ya kiserikali ya Truya wamesema ili kuondokana na machafuko yanayoweza kusababisha uvunjifu wa amani, viongozi wanaokiuka matakwa ya uongozi, uvunjaji wa Katiba na sheria za nchi wanapaswa kuwajibishwa kwa mujibu wa sheria.
Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Helman Sheluleta alisema Ibara ya 18 ya Katiba ya nchi inatambua haki ya mtu kutoa maoni, kusikilizwa na kuandamana kwa amani na kwa mujibu wa sheria lakini sheria inapovunjwa kwa ajili ya kupata haki ndiko kuhatarisha amani ya nchi.
No comments:
Post a Comment