Saturday, March 12, 2011

waandishi wambana spika makinda

KAULI ya Spika kutaka wabunge wasome magazeti kama barua, imemtia matatani baada ya waandishi wa habari jana kumtaka awaombe radhi kwanza, ili watekeleze ombi lake la kuvitaka vyombo vya habari, viwe kiungo kati ya Bunge na wananchi.

Hata hivyo Spika Anne Makinda, aligoma kuomba radhi na kwamba alitoa kauli hiyo katika mazingira ambayo, hakuamini kama vyombo vya habari vingeweza kutoa taarifa aliyodai kuwa haikumtendea haki.

Katika mkutano wa pili wa Bunge la Kumi mjini Dodoma, Makinda aliishambulia makala iliyoandikwa na gazeti hili kuhusu mabadiliko ya kanuni za Bunge, zilizogusa kambi ya upinzani bungeni ambayo wabunge waliitumia kama marejeo, akisema "magazeti yasomwe kama barua".

Lakini jana akifungua semina ya siku mbili ya waandishi wa habari za Bunge, makinda alibanwa na waandishi wakimtaka aombe radhi muda mfupi baada ya spika huyo kueleza kuwa vyombo vya habari, ni nguzo muhimu na kiungo kati ya Bunge na wananchi.

"Mheshimiwa spika leo umetaka vyombo vya habari viwe kiungo kati ya Bunge na wananchi, lakini katika Bunge lililopita uliwataka wabunge wasome magazeti kama barua ukimaanisha hayana umuhimu, unaweza kufuta kwanza kauli hiyo au kuomba radhi kabla hatujatekeleza ombi lako,," alihoji mmoja wa washiriki wa semina hiyo.


Akionekana kutaharuki Spika Makinda alijibu,"nilijua ntakumbana na swali hili na nimejiandaa vema, sio kuomba radhi bali kutoa ufafanuzi."Nilifedheheshwa na habari ile, waliandika kinyume na ilivyo, walisema mimi ninakandamiza upinzani. Hapana mimi natakiwa kutoegemea upande wowote kwani nikitenda yaliyoandikwa naweza kuvuruga amani ya nchi. Spika peke yake anaweza kuvuruga amani ya nchi," alisema

Spika Makinda alifafanua kuwa kilichofanyika haikuwa kubadili kanuni za Bunge bali kutafsiri.

"Tulitafsiri kanuni ya 14(2) ambayo inasema kambi rasmi ya upinzani inaundwa na wabunge wote wa upinzani. Zamani ilikuwa kambi rasmi ya upinzani inatengenezwa na asilimia 30 ya wabunge, lakini hili halijawahi kutekelezeka kwa kuwa mwaka 1995 wabunge wa upinzani walikuwa 46 ambao ni chini ya asilimia 30 na mwaka 2000 hawakufikia hata asilimia 2. Bunge likalazimika kubadilisha kanuni na kuwa asilimia 12.5 ya wapinzani inaweza kuunda upinzani," alifafanua.

Lakini akitoa mada katika semina hiyo mwandishi nguli wa habari, Jenerali Ulimwengu, alisema kuwa kauli ya Spika kutaka wabunge wasome magazeti kama barua ni makosa."...Kwa maoni yangu Spika Makinda aliposema wabunge wasome magazeti kama barua alikosea," alisema Ulimwengu.Katika semina hiyo Spika Makinda alisema kuwa kanuni za Bunge zitafanyiwa mabadiliko makubwa katika kipindi hiki cha bunge la kumi.

"Tunaenda kufanya mabadiliko makubwa ya kanuni, na hivyo kambi rasmi ya upinzani haitakuwa tena issue ya kuumiza kichwa..," alisema Makinda.Alisema pia kwamba katika Bunge lijalo Sheria ya Vyombo vya Habari inatarajiwa kufikishwa bungeni tayari kujadiliwa na kwamba wadau watapata nafasi ya kushiriki katika mijadala yake.

Kuhusu Katiba, Makinda alisema mchakato huo ni muhimu na kwamba vyombo vya habari vina nafasi kubwa katika kuwaelimisha na kuwapa taarifa wananchi kuhusu mabadiliko hayo ili nao washiriki katika uandikaji katiba hiyo mpya.

No comments:

Followers