Friday, December 19, 2008

Profesa Wangwe ashangaa serikali kununua mashangingi badala ya kompyuta


MHADHIRI mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Samuel Wangwe amehoji matumizi mabaya ya fedha za serikali ambayo yamesababisha nchi kubaki nyuma katika sekta ya mawasiliano na ugunduzi.
Akizungumza juzi katika semina ya maandalizi ya mapitio ya Mpango wa Taifa wa Sayansi, Teknolojia na Ugunduzi (NIS) iliyofanyika mjini Bagamoyo iliyoandaliwa na serikali kwa ushirikiano na Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi (UNESCO), Prof Wangwe alisema inashangaza kuona idara nyingi na wakala kadhaa wa serikali zikiwa hazina vitendea kazi vya kisasa kama kompyuta, huku wizara hizo hizo zikiwa na magari mengi ya kifahari maarufu kama mashangingi.
“Inanishangaza sana ninapopita katika baadhi ya idara za serikali na kukuta hazina kompyuta wala intaneti wakati tupo katika zama za sayansi na teknolojia na halafu eti idara hizo hizo zina ‘mashangingi’ mengi hata wakati mwingine hayahitajiki,” alisema.
“Hivi tukiangalia kwa umakini ‘shangingi’ moja linanunua kompyuta ngapi, kwa makadirio ya urahisi, ‘shangingi’ moja linanunua kompyuta 60 mpaka 100, na hizi kompyuta zikitumika vizuri zinaweza kuongeza ufanisi katika serikali na kwingineko kote na kuwezesha kununua ‘mashangingi’ mengine mengi tu.”
Alisema serikali inaweza kupiga hatua katika nyanja za mawasiliano, teknolojia na ugunduzi iwapo kunakuwapo utashi wa kisiasa na mapinduzi ya fikra katika mipango mbalimbali hususani ya bajeti.
Wazo hilo liliungwa mkono na wadau mbalimbali waliohudhuria semina hiyo akiwemo mkurugenzi wa mawasiliano hifadhi za nyaraka wa tume ya sayansi na teknolojia- COSTEC, Theophil Mlaki ambaye aliigeukia jamii na kutaka kuwwepo mkakati wa makusudi wa kuiwezesha kubadilika kuwa ya kisayansi.
''Tanzania tuna ng’ombe milioni 30 lakini ng'ombe hawa wanachangia asilimia nne ya pato la taifa, lakini simu za mkononi ziliingia juzi tu hapa nchini na ambazo kampuni zake zina wateja karibu milioni 10 , zinaliingizia taifa zaidi ya asilimia 20 hivi kwanini tusijenge jamii ya kisayansi kuweza kuwatumia ng'ombe wetu tukafaidika nao, kuliko ilivyo sasa,'' alisema.
Naye mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMRI), Dk. Andrew Kitua alitaka kuwepo uhusiano mzuri kati ya ugunduzi wa kisayansi unaofanyika na ongezeko la kipato la taifa au jamii husika ili kuwe na maendeleo ya uhakika.
Akifunga semina hiyo, Mkurugenzi wa Sayansi na Teknolojia katika wizara ya sayansi, mawasiliano na teknolojia, Profesa Evelyne Mbede alisema wizara yake iko katika hatua za mwisho za kukamilisha mapitio ya sekta hiyo ili kuweza kuanzisha mradi wa sayansi teknolojia na ugunduzi utakaotekelezwa kwa miaka miwili na nusu na utakaoligharimu taifa Sh13bilioni kwa ushirikiano na Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi (UNESCO).

No comments:

Followers