Tuesday, December 16, 2008

WANANCHI KUSHIRIKISHWA KATIKA KUHIFADHI MALI ASILI

Wizara ya Maliasili na Utalii imeanzisha mpango wa ushikirishaji wa wananchi katika rasilimali za maliasili, malikale na utalii kwa lengo la kutoa elimu ya uhifadhi wa misitu na maliasili kwa jamii. Waziri wa Maliasili na Utalii.

Shamsa Mwangunga aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akifungua semina ya siku mbili iliyoandaliwa kwa wahariri wa vyombo vya habari kwa lengo la kutoa msukumo wa umuhimu wa hifadhi za maliasili na kujadili mikakati iliyofikiwa na wizara hiyo katika utekelezaji wa sera mbalimbali.
Mwangunga alisema wizara imefanya jitihada nyingi ili kuleta maendeleo katika hifadhi za maliasili na malikale, ingawa elimu ya kutosha haijatolewa kwa wananchi juu ya umuhimu na faida ya kuhifadhi maliasili zilizopo nchini. Aliwapa changamoto wahariri hao kuangalia eneo la misitu na nyuki na mambo ya kale, kwa sababu ni moja ya idara ambazo rasilimali zake hazijaweza kutambulika ipasavyo kwa wananchi na kama watazifahamu vya kutosha, zitawasaidia katika kuinua kipato chao kupitia mali kama asali.
Aidha, alivishukuru vyombo vya habari kwa kazi nzuri vinayofanya kuandika taarifa za wizara hiyo, ziwe kwa mtazamo chanya au hasi, na kueleza kuwa taarifa hizo zimekuwa chachu ya kuleta mabadiliko katika wizara hiyo.
Mmoja wa watoa mada, Mkurugenzi wa Sera na Mipango katika Wizara hiyo, James Lugaganya alisema kwa upande wa rasilimali ya nyuki, Tanzania ina uwezo wa kuzalisha tani 138,000 za asali na tani 9,200 za nta kwa mwaka. Pia alisema ufugaji nyuki huchangia katika maendeleo ya jamii kuinua uchumi wao na kuhifadhi mazingira hususan misitu kwa lengo la kuondoa umasikini. Alisema katika kutekeleza sera ya ushirikishaji, Idara ya Misitu na Nyuki inalenga katika kuwashirikisha wananchi katika kuboresha misitu iliyopo kwenye maeneo yao, vilevile kuanzisha hifadhi mpya za misitu vijijini, kupanda miti kwa wingi zaidi ya matumizi pamoja na matumizi wa majiko banifu na nishati mbadala. Aidha, amewatia moyo wananchi, akisema wizara ina matarajio ya kuweka mipango mizuri ya uhifadhi pamoja na kuwawezesha wananchi wengine hususan kujiondolea umasikini kwa kutumia maliasili zilizopo nchini.

No comments:

Followers